Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC) Kupitia Mrajis Msaidizi wa Mkoa wa Shinyanga kwa kushirikiana na Vyama vikuu Vya ushirika vya Mkoa wa Shinyanga Kahama Cooperative Union (KACU LTD) na Shinyanga Region cooperative Union (SHIRECU LTD) wameandaa jukwaa la Maendeleo ya Ushirika Mkoa wa Shinyanga lililofanyika tarehe06 Marchi 2023, Katika viwanja vya Chuo cha Ushirika Moshi (MoCU) tawi la Kizumbi Manispaa ya Shinyanga, huku Mgeni Rasmi akiwa ni Kaimu Naibu Mrajis Uratibu na Uhamasishaji kutokaTume ya Maendeleo na Ushirika Tanzania (TCDC) Bi Consolata Kiluma.
Lengo kuu la jukwaa hili ni kujadili changamoto mbalimbali na kuzitafutia ufumbuzi ili kuviimarisha vyama vya Ushirika katika Mkoani Shinyanga.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa jukwaa hilo, Mgeni rasmi Bi. Consolata Kiluma amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan pamoja na wasaidizi wake, Mhe Dkt Philipo Mpango (Makamu wa Rais), Mhe Kassim Majaliwa Kassim (Waziri Mkuu) (Mb) na Mhe. Hussein Mohamed Bashe (Waziri wa kilimo) (Mb) kwa kazi kubwa inayofanywa na serikali ya awamu ya sita kupitia wizara ya kilimo na hasa kwenye kuimarisha vyama vya ushirika ambavyo ndivyo mkombozi wa mkulima.
Amesema Ushirika kwa sasa unafanya vizuri tofauti na miaka michache iliyopita, kutokana na viongozi wakuuu wa nchi kuwekeza nguvu nyingi katika kilimo na ushirika na kuhakikisha Ushirika unaendelea kusimama imara.
“Katika kuendelea kuimarisha vyama vya Ushirika mkoani Shinyanga napenda kusisitiza mambo machache, viongozi wa vya vyama vya Ushirika mnachangamoto ya kutokufuata Sheria ya vyama vya Ushirika namba 6 ya mwaka 2013, pamoja na Kanuni zake za mwaka 2015 na Sheria ya huduma ndogo ya fedha ya mwaka 2018 na kanuni zake za mwaka 2019,”alisema Kiluma.
“Viongozi mkifuata Sheria hizi mtaendelea kuimarisha vyama vya ushirika, pia mnapaswa kuwa waadilifu, waaminifu ili kurudishataswira nzuri ya vyama vya Ushirika, pamoja na kutangaza mambo mazuri ambayo mnayafanya ndani ya jamii” aliongeza Kiluma.
Aidha, alisema Jambo jingine ambalo linapaswa kufanyiwa kazi na viongozi wa vyama vya Ushirika, ni kujibu hoja za ukaguzi kutoka kwa Mkaguzi wa vyama vya Ushirika ili vyama vipate viweze kupata hati Safi.
Naye Mkaguzi wa nje wa Vyama vya Ushirika kutoka shirika la ukaguzi COASCO Mkoa wa Shinyanga, CPA Rodrick Kilemile, alisema katika ukaguzi ambao wameufanya mwaka (2021-2022) kwa vyama vya Ushirika 237, vyama vilivyopata Hati safi ni Saba (7), Hati yenye Shaka hamsini na moja (51), Hati isiyoridhisha vitatu (3) na Hati chafu vyama mia moja sabini na sita (176).
Kwa upande wake Mrajis Msaidizi wa vyama vya Ushirika mkoani Shinyanga Bi. Hilda Boniphace, alisema mikakati ambayo wamejiwekea katika msimu ujayo ni kuhakikisha vyama vya Ushirika zaidi ya 153 vinapata Hati safi.
Alisema katika ukaguzi ambao wameufanya kwenye vyama vya Ushirika 51, ambapo vyama 45 ni vya mazao, 6 vya akiba na Mikopo ikiwa ni ukaguzi wa kawaida, na ukaguzi maalumu wameufanya kwa vya 6, na kubaini tatizo la kutozingatiwa makisio yaliyoidhinishwa na Mrajis, Bodi ya chama kukaa Madarakani muda unaopita kiasi, uandishi mbovu wa vitabu, na kukosekana kwa vitabu vya fedha.
“Changamoto ambayo tumeibaini inasababisha upatikanaji wa hati zenye shaka kwenye vyama vya mazao, ni vyama kutofuta madeni ya nyuma, na tumejipanga dosari zote hizi tunaziondoa kwa kufuta madeni ili tutoke kwenye hati zenye Mashaka na kupata Hati Safi ”alisema Bi Hilda Boniphace.
Pia alitaja baadhi ya changamoto ambazo zinakabili Ushirika Mkoa wa Shinyanga, ni uzalishaji mdogo wa mazao, uongozi kutofuata misingi ya utawala bora, kufanya kazi kimazoea, mipasuko kwenye bodi za Vyama na kuvuruga wana Ushirika, pamoja na kuacha kusimamia malengo yaliyokusidiwa kusajili chama, pamoja na watendaji kukosa Sifa na weledi.
Alitaja baadhi ya mafaniko kuwa ni kukagua vyama vya Ushirika 51 licha ya kukabiliwa na upungufu wa Maafisa Ushirika kwani Mkoa mzima wapo maafisa ushirika 8 tu na walipaswa wawe 20.
Alisema pia wametoa mafunzo kwa viongozi 450 na watendaji 174, na kutekeleza mfumo wa uuzaji wa mazao na kuvisajili vyama 261, na kuingiza kwenye mfumo makisio ya vyama 13 vya akiba na mikopo, pamoja na kuendelea kutekeleza miongozo iliyotolewa na Tume ya Maendeleo ya Ushirika.
Jukwaa hilo lilienda Sambamba utoaji wa tuzo kwa vyama vya Ushirika vilivyofanya vizuri ambapo chama cha msingi Ngokolo 2001 kutoka Kahama kilipata tuzo ya chama bora katika utunzaji wa kumbukumbu, usimamizi bora na chama pamoja na kupata hati safi ya ukaguzi kwa miaka miwili mfululizo na Menejimenti ya KACU LTD ilipata tuzo ya menejimenti bora ya Vyama vikuu vya Ushirika Mkoa wa Shinyanga.
No Comments